Mokiwa Chedy Dominic

Think big, act simple. Happiness is hidden in simple things

About

Our mission is to help people discover the hidden treasure in doing small acts of kindness. Health is capital, and health is built by considering the smallest things. Think big, act simple. Happiness is hidden in simple things.

Usalama wa Chakula: Jinsi Ya Kujikinga na Magonjwa Yaenezwayo kwa Vyakula

Mwanadamu hula kwa wastani tani 70,000 za chakula katika kipindi cha uhai. Hutumia muda wa miaka tisa na miezi minne kwa kula. Pia mwanadamu hupaswa kuchagua kati ya aina 100,000 za chakula katika kipindi chote cha uhai wake. Kibaya zaidi ni kwamba wengi huishia kula vyakula vya aina moja. Hali hii inasababishwa hasa na uelewa mdogo kuhusu elimu ya lishe. Pia, umasikini unachangia.

Miongoni mwa vyakula vinavyoliwa kwa kiasi kikubwa ni vyakula vya nafaka, mboga mboga, nyama, maziwa na matunda pamoja na mizizi. Jambo kubwa la kuzingatia ni kwamba chakula kimoja hakiwezi kuwa na virutubisho vyote. Hapa ndipo maana halisi ya chakula ni sanaa inapopatikana. Chakula huhitaji umakini katika uchaguzi na uandaaji wake. Hili huhitajika ili kumvutia mlaji na kumfaa kiafya.

Uchaguzi wa chakula na aina ya mapishi ni sanaa muhimu katika kumfanya mlaji afurahie.

Unapofanya uchaguzi wa chakula basi fanya yafuatayo:-

  • Chagua kwa kuzingatia rangi ya chakula. Inapendekezwa kuwa ni vizuri rangi zote za upinde wa mvua ziwakilishwe katika mlo mmoja.
  • Zingatia hali ya ugumu na ulaini. Kwa masaa ya usiku, si vyema kula chakula kigumu. Chagua chakula kinachomeng’enywa kwa urahisi.
  • Chagua kwa kuzingatia radha
  • Katika kuchagua chakula, hakikisha hutumii chakula cha aina moja hata kikakukinai. Kurudia chakula sana ni sumu
  • Chakula kiwe rahisi, cha kuvutia kisicho na viungo vingi vinavyopoteza radha halisi

Mchanganyiko wa chakula ni budi uhusishe vyakula kutoka katika makundi yote ya vyakula. Chagua chakula chenye lishe kwa wingi na si chenye nguvu nyingi. Hii hutegemea zaidi umri, aina ya kazi unazofanya na hali tu ya kiafya. Kwa mfano, mtu anayefanya kazi za kutumia nguvu sana anahitaji chakula cha wanga cha kutosha. Mtu anayebeba vyuma au mtunisha misuli anahitaji protini na wanga ya kutosha pia.

Pia katika uandaaji, tulisisitiza katika somo lililopita kuwa, tunapaswa kutumia vyakula vya nafaka isiyokobolewa. Asilimia themanini ya viini lishe huondolewa wakati wa kukoboa chakula. Hivyo chakula kilichokobolewa ni makapi tu yenye sukari nyingi lakini yenye upungufu mkubea wa viini lishe. Bonyeza link hii kwa somo lililopita: https://mokiwa.blog/2024/10/21/vyakula-vya-wanga-na-maandalizi-yake/

Mtu anapaswa kuwa makini asitumie tu vyakula bila malengo. Lazima ahakikishe anachagua vyakula vyenye maana mwilini kwa umakini mkubwa. Epuka sana vyakula vifuatavyo:

  • Vyakula vyenye mafuta mengi kama vile siagi, jibini. Epuka hasa matumizi ya mafuta ya wanyama.
  • Vyakula visivyosanifiwa au vilivyozindikwa viwandani. Vyakula vya viwandani hutumia aina Fulani za kemikali za kutunzia vyakula ili visiharibike. Kama itakulazimu, basi tumia vyakula vilivyokaa kwa muda mfupi na ule kwa kiwango kidogo tu.
  • Vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta. Kiwango cha mafuta katika vyakula vilivyokaangwa ni kikubwa sana. Kumbuka tunapaswa kukwepa chakula chenye mafuta mengi. Hii ni kwa ajili ya kulinda usalama wa miifumo ya damu, moyo na kadharika.
  • Epuka vyakula visivyo na lishe au nguvu ndani yake kama vile kahawa, vinywaji vyenye caffeine, pombe nakadharika.

Ni jambo linalopaswa kuzingatiwa kuwamba; Chakula unachokula ni sharti kiwe katika mringanyo sawa na shughuli au kiwango cha mazoezi unayofanya. Haupaswi kukaa bila kufanya mazoezi yoyote. Kufanya mazoezi kutakuepusha na magonjwa yatokanayo na ulaji mbaya. Magonjwa haya ni kama vile shinikizo la juu ya damu, magonjwa ya moyo, na kuwa na kiwango kikubwa cha uzito. Pia, maumivu ya viungo yanaweza kutokea kwa sababu ya uzito mkubwa.

Hupaswi kuishi bila kufanya mazoezi. Mazoezi hutuepusha na magonjwa mbalimbali yatokanayo na uvivu.

Kiwango cha nguvu kinachopatikana kwenye chakula unachokula kiwe sawa na kiwango kinachotoka kwa njia ya mazoezi.

Usalama wa chakula

Huenda umekumbana na haya: Maumivu ya misuli au kujihisi kizunguzungu. Uchovu, maumivu ya tumbo, au kujihisi baridi au homa. Kuhara au tumbo kusokota na kuishiwa nguvu mwilini. Pia, maumivu ya kichwa na kichefuchefu. Mambo haya huenda uliyachukulia kama ya kawaida kwako.

Yapo mambo ambayo huhitaji umakini wa haraka yanapokutokea. Baadhi ya dalili ni kuonekana kwa damu katika kinyesi na kuhara kwa zaidi ya siku tatu. Dalili nyingine ni kuona maruweruwe (double vision) au shida katika kumeza chakula. Homa kwa zaidi ya siku tatu pia ni dalili ya kushughulikiwa. Dalili zingine ni ganzi au mnyeo (msisimko), pamoja na mapigo ya moyo kwenda haraka na unyonge au udhaifu wa mwili.

Endapo matatizo tajwa hapo juu hayatashughulikiwa kwa haraka, yanaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu. Haya ni kama vile kuishiwa kwa maji au damu mwilini. Tatizo linguine ni kushuka kwa kinga ya mwili. Pia, kuna tatizo la unyonywaji wa chakula katika utumbo kutokana na usagaji mbaya wa chakula (Malabsoption). Pia, yanaweza kusababisha utapiamlo na kifo. Matatizo mengi hutokana na usalama mdogo wa chakula.

Miongoni mwa vitu vinavyotishia usalama wa chakula ni pamoja na sumu katika vyakula au uchafu. Sumu katika vyakula hupelekea mtu kutapika, kuharisha na kadharika. Chanzo kikuu cha sumu hizi ni pamoja na vijidudu kama vile bacteria, virus, minyoo pamoja na kuvu. Vyanzo vya wadudu hawa ni hewa na maji yasiyo salama. Chakula yenyewe, kwa mfano chakula kilichochacha, pia ni chanzo. Wanyama wa kufugwa au wa mwitu na chawa pia ni vyanzo vya wadudu hawa.

Nafaka nyingi kama vile karanga, mihogo na mahindi huathiriwa na kuvu. Kuvu huzalisha sumu-kuvu inayoathiri hasa mfumo wa fahamu.

Katika nchi zinazoendelea, kwa kila dakika sita mtoto mmoja hufa kwa kuhara. Wanne kati yao husadikika kuwa wametumia chakula au maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu.

Wapo wadudu wadogo na wanaopendeza kwa kuwaangalia katika hadubini lakini wenye athari kubwa sana wanapopata fursa ya kuingia mwilini. Athari zake ni pamoja na kifo. Wadudu hao wanapopata fursa ya kuingia katika mwili wa binadamu au wanyama wengine tunaofuga, huleta madhara makubwa ssana kiafya.

Mifano ya wadudu hatari katika Vyakula

  • Salmonella sp.- Bakteria hawa husababisha homa ya matumbo. Kwa ncha ndogo ya sindano, unaweza kubeba wadudu wa aina hii. Kiasi cha milioni moja ya wadudu hawa hawaonekani kwa macho ya kawaida.
  • Hepatitis virus- Virusi hivi husababisha homa ya ini. Ncha ya sindano ya kushonea nguo huweza kubeba kiasi cha wadudu bilioni moja pasipo kuonekana kwa macho.
  • Protozoa (Ameba, Giardia, Flukes)- Minyoo hii isiyoonekana kwa macho tupu huweza kubebwa kwa ncha ya pini bila kuonekana. Ncha ndogo ya pini huweza kubeba minyoo mitano bila kuonekana kwa macho. Huchukua masaa 12-36 kuanza kuleta madhara mwiwlini. Wadudu hawa hupatikana katika maji ya madimbwi, nyama, mazao ya kwenye maji na kadharika.
  • Clostridium botulinum. Bakteria huyu hupatikana katika Mbogamboga za kwenye makopo, nyama au katika mazingira ya asili. Huhitaji kati ya masaa 1-6 kuanza kuleta amadhara mwilini.
  • Staphylococcus. Bacteria hawa tunao katika mazingira yetu karibia yote yaani maji na hewa. Inapotokea umekula chakula kilicho na wadudu hawa, basi huchukua masaa 4-5 madhara yaake kuanza kuonekana.

Wadudu wengi tuko nao katika mazaingira ya nje na ndani ya mwili (normal floras). Hutokea pia wakaingia mwilini kwa njia mbalimbali. Hivyo, huleta athari mwilini.

Mwonekano wa bacteria aina ya Clostridium botulinum katika hadubini. Bakteria huyu huzalisha sumu aina ya botulinum ambayo hudhuru neva za fahamu na kusababisha kiharusi.

Kuwa na wadudu hawa haimaanishi kuwa ni mgonjwa. Ila utakuwa mgonjwa kwa kuangalia: aina ya vijidudu, kiasi cha vijidudu au kiwango cha sumu. Kiasi cha chakula au maji yaliyotumika, uwezo wa kinga na kiwango cha mafuta katika chakula (water activity).

Yapo mazingira yanayochochea ukuaji na uzalianaji wa haraka wa vimelea ambayo kwayo tunaweza kutumia kujilinda dhidi ya madhara yao. Vifuatayo ni vitu vinavyowasaidia wadudu wa maradhi kukua. Ni budi ikumbukwe kwamba mahitaji yao hutofautiana.

Ili wadudu wakue na kuleta madhara huhitaji:

  • Muda. Kati ya masaa 0-4 vimelea huongezea toka 1,000- 4,000,000 katika nyama. Hivyo nyama haipaswi kuachwa wazi kwa muda mrefu.
  • Unyevu katika chakula au mwili. Maji maji huhitajika ili kumfanya mdudu akue na kuleta madhara. Epuka unyevunyevu katika mwili, mavazi na chakula.
  • Wadudu pia huhitaji jotoridi mahususi. Chakula kinapotunzwa katika hali ya unyevu na jotoridi linalomfaa mdudu husika, basi kitaharibiwa na kitakuharibia afya utakapokitumia. Kwa mfano panapokuwa na unyevu na joto la wastani, fungasi huvamia chakula na kukua kwa haraka sana.
  • Wadudu huhitaji kiwango cha alkali stahiki yaani ph. Wapo wadudu wanaokuwa kwa haraka katika hali ya aside, wengine katika alkali na kadharika. Jua aina ya chakula chako.
  • Wadudu huhitaji chakula. Kiwango cha lishe wanayoihitaji mfano sukari, madini, vitamin. Kama unaumwa tumbo na unahara usitumie vyakula vya sukari. Kutumia sukari wakati unahara, ni kuendelea kuwalisha wadudu hivyo watazaliana kwa wingi na kukudhuru zaidi.

Makundi Ya Watu Walio Katika Hatari Zaidi

Si makaundi yote huathiriwa na matumizi ya vyakula. Hii hutegemea sana kinga ya mtu husika. Lakini yapo makundi ambayo huathiriwa kwa urahisi sana wanapotumia chakula kisicho na usafi wa kutosha.

  • Watoto wadogo hasa wanaonyonya, kutambaa au hata kutembea. Hii ni kwa sababu ya mazingira wanakocheza yana wadudu waletao maradhi. Wadudu kama vile bakteria, virus na minyoo wako katika mazingira tunayoishi. Inashauriwa kutumia dawa za minyoo kwa kila baada ya miezi mitatu. Ni jambo la kuaminika kuwa kila mtu ana minyoo kwa maana wanapatikana katika vyakula tunavyokula hasa matunda.
  • Kundi jingine ni kina mama wajawazito. Tatizo huweza kusababishwa na ulaji wa udongo usio salama kipindi cha ujauzito.
  • Kundi la tatu ni watu walio na kinga hafifu au duni ya mwili. Kwaw mfano mtu mwnye maambukizi ya virusi vya ukimwi, hushambuliwa sana na magonjwa nyemelezi kwa sababu ya kinga yake kutokuwa na uwezo wa kuhimili maambukizi

Jinsi Ya Kujikinga Na Magonjwa Katika Vyakula

  • Osha mikono kwa maji safi yanayotiririka pamoja na sabuni kabla ya kula hasa unapotoka maliwato.
  • Osha mikono kabla ya kuanza kuandaa chakula chochote.
  • Kunywa maji safi yaliyochemshwa, yaliyochujwa na kutunzwa mahali salama kwa maana kuchemsha maji si kinga kwamba hayatachafuliwa hivyo chombo kinachotumika kuchotea kisitumike kunywea. Weka uangalizi kwa watoto kujichotea maji, ikiwezekana watoto wadogo wasiruhusiwe kujichotea maji ya kunywa.
  • Safisha kinywa kwa maji safi na dawa kuzuia minyoo kama vile Amoeba
  • Safisha vyombo au mahali pa kupikia kabla au mara baada ya kuvitumia. Visiachwe vikachezewa na mifugo ya nyumbani au wadudu warukao kama nzi.
  • Tumia chakula kingali cha moto kuzuia kuchafuliwa na wadudu walio hewani (wengine hutokana na mazungumzo wakati wa kula au kupakua).

Ifahamike kuwa, bakteria hawafi katika joto la jokofu bali hujifungia kusubiri joto. Bakteria  huweza kukaa katika hali ya ubaridi kwa muda mrefu hata milele bila kufa. Mazao ya wanyama yasiachwe katika jotoridi la mazingira (room temperature) kwa muda zaidi ya masaa mawili. Yasikae kwa saa nzima katika mazingira ya joto.

Kuvu jamii ya penicillium na cladosporium ni miongoni mwa wadudu wanaoweza kuishi katika baridi jokofu. Huzalisha sumu-kuvu inayoathiri mfumo wa fahamu. Si salama kutunza chakula katika jokofu bila kufunika.

Tahadhari Kwa Vyakula Ghafi

Vyakula kama vile matunda vingi havipikwi, hii ni pamoja na mboga ambazo hazipaswi kukaa muda mrefu katika moto. Fanya yafuatayo:-

  • Sugua na safisha matunda na mboga za majani kwa maji safi yanayotiririka
  • Menya matunda inapobidi kwa kutumia kisu safi na kwa haraka. Ussiyaache wazi kwa muda mrefu kuepuka wadudu walioko katika hewa.
  • Epuka kushikana mikono, kujikuna wakati unaandaa au kula.
  • Usitumie sabuni kuosha mboga au matunda
  • Kuna matunda huwa yana vidonda kwa mfano mahali palipoanza kuoza. Ondoa mahali palipo na kidonda maana ndipo wadudu walipo kwa wingi.

Tunza chakula katika vyombo visivyoruhusu hewa kupenya. Tumia chupa au vifaa maalum visivyopasuka. Usiruhusu vifaa hivyo kutobolewa na wadudu au wanyama kama panya. Weka katika jokofu vyakula vikiwa vimefunikwa au kufungwa. Kumbuka wapo bakteria wanaohitaji ubaridi sana ili kuishi, kumbuka pia baridi haiui bakteria bali moto. Suala la kutunza vyakula katika jokofu lifanyike kwa muda mfupi. Tunza vyakula vikavu mahali tulivu, penye giza, safi na kwa kuvifunika katika joto kati ya nyuzi-joto 10-21. Punguza uwazi, utunzaji au ubebaji usio na wa lazima.


Discover more from Holistic Health and Nutrition

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply

Discover more from Holistic Health and Nutrition

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Discover more from Holistic Health and Nutrition

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading